 |
Bustani ya 'Independence Square' katika Manispaa ya Dodoma inavyoonekana kwa sasa ikiwa imezungukwa na wafanyabiashara ndogo. |
 |
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme (katikati) akikata utepe kuashiria ufunguzi Rasmi wa Bustani ya 'Independence Square' katika Manispaa ya Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Juni 5. Kushoto ni Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede na kulia ni Meneja wa Benki ya Akiba inayohudumia Bustani hiyo John Magigita. |
 |
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya hafla ya Ufunguzi |
 |
Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa hafla hiyo |
 |
Ofisa Mazingira na Usafishaji wa Manispaa ya Dodoma Dickson Kimaro aliyemuwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi akijibu maswali kutoka kwa Waandishi wa Habari wakati wa Hafla hiyo. PICHA ZOTE NA RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI MANISPAA YA DODOMA |
MKUU wa Wilaya ya
Dodoma Christine Mndeme amesema wafanyabiashara ndogo waliozunguka eneo la
bustani ya Uhuru katika Manispaa ya Dodoma wataondolewa na kuhamishiwa katika
masoko ya Sabasaba na Bonanza ili eneo hilo libaki wazi kwa ajili ya kuupezesha
mji wa Dodoma na kuufanya uvutie zaidi ili kufikia lengo la kuboreshwa kwa
bustani hizo.
Alitoa ahadi hiyo
alipokuwa akifungua rasmi bustani hiyo leo Juni 5, 2017 ikiwa ni sehemu ya
maadhimisho ya kilele cha Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika
viwanja vya ‘Nyerere Square’ Manispaa ya Dodoma.
Bustani hiyo inahudumiwa
na Benki ya Biashara ya Akiba (ACB) kwa makubaliano maalum na Manispaa ya
Dodoma, ambapo meneja wa tawi la Benki hiyo John Magigita imeeleza kuwa
changomoto kubwa ni kuwabustani hiyo imezungukwa na wafanyabiashara ndogo hali
inayopelekea kupoteza mvuto wake na kutoonekana vizuri.
Naibu Meya wa
Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede amesema Manispaa ya Dodoma itashirikiana na
Ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya katika kuwahamisha wafanyabiashara hao na
kutafutia nafasi katika masoko mengine baada ya soko la majengo kujaa hali
iliyopelekea wao kupanga bidhaa zao katika viunga vya bustani hiyo.
Naye Ofisa Mazingira na Usafishaji
wa Manispaa ya Dodoma ambaye
alimuwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi katika Hafla hiyo
fupi ya ufunguzi, alisema kuwa Manispaa imejipanga kuhakikisha mji wa Dodoma
unakuwa katika hali ya usafi muda wote kwani tayari Dampo jipya la kisasa la
kuzika taka lililopo katika eneo ya Chidaya limeshaanza kazi na kwamba
watendaji wa Kata watashirikishwa kikamilifu katika kusimamia sheria za usafi
na mazingira katika maeneo yao.