....................................................................
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amekabidhi hundi ya Shilingi Milioni 950 zilizotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutoka katika Mfuko wa Wanawake, Vijana, na Walemavu kwa ajili ya vikundi 234 vya Wanawake na Vijana huku akitoa wito kwa Jiji hilo kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa na vikundi hivyo kwani imekuwa moja ya changamoto zinazowakabili katika shughuli zao.
Hafla
ya kukabidhi hundi hiyo kwa Wanavikundi hao imefanyika hivi karibuni katika
Viwanja vya Nyerere vilivyopo katikati ya Jiji la Dodoma.
‘’Viongozi muandae Mpango Mkakati wa kuwa na
masoko ya kuuza bidhaa za wajasiriamali hawa, nimeona wana bidhaa nzuri sana
ambazo unaweza usiamini kama zinatoka Dododma, lakini kila mmoja ukimuuliza
soko anakwambia hana soko maalumu’’ Alisema Waziri Jafo.
Aliongeza ‘’Mbali
na kuwapa fedha lakini pia nakuagiza Mkurugenzi wa Jiji (Godwin Kunambi ) na
Mstahiki Meya (Profesa David Mwamfupe) mtafute eneo la kimkakati kwa ajili ya hawa
mnaowapatia mkopo na vikundi vyote vilivyowezeshwa na Halmashauri hii, kwa
kufanya hivi tunaweza kuwa na eneo moja maalumu ambalo litakuwa linafanya
maonyesho kwa mwaka mzima’’ Alisema.
Awali,
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi alimweleza Waziri Jafo kuwa, fedha
hizo zinatokana na ukusanyaji bora wa mapato ya ndani na kwamba kwa sasa
Halmashauri inatoa mikopo mikubwa kuanzia Shilingi milioni moja hadi milioni
kumi na kutoa wito kwa wajasiriamali kujiunga katika vikundi vya kiuchumi ili kukidhi
vigezo vya kupata mikopo hiyo.
Alisema
fedha hizo zinatolewa kwa vikundi 234 vya Wajasiriamali, vikiwemo 168 vya Wanawake
pamoja na vikundi 66 vya Vijana.