Monday, June 5, 2017

WAFANYABIASHARA BUSTANI YA UHURU KUONDOLEWA



Bustani ya 'Independence Square' katika Manispaa ya Dodoma inavyoonekana kwa sasa ikiwa imezungukwa na wafanyabiashara ndogo.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme (katikati) akikata utepe kuashiria ufunguzi Rasmi wa Bustani ya  'Independence Square' katika Manispaa ya Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Juni 5.  Kushoto ni Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede na kulia ni Meneja wa Benki ya Akiba inayohudumia Bustani hiyo John  Magigita.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya hafla ya Ufunguzi
Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa hafla hiyo
Ofisa Mazingira na Usafishaji wa Manispaa ya Dodoma Dickson Kimaro aliyemuwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa  hiyo Godwin Kunambi akijibu  maswali kutoka kwa Waandishi wa Habari wakati wa Hafla hiyo. PICHA ZOTE NA RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI MANISPAA YA DODOMA



MKUU wa Wilaya ya Dodoma Christine Mndeme amesema wafanyabiashara ndogo waliozunguka eneo la bustani ya Uhuru katika Manispaa ya Dodoma wataondolewa na kuhamishiwa katika masoko ya Sabasaba na Bonanza ili eneo hilo libaki wazi kwa ajili ya kuupezesha mji wa Dodoma na kuufanya uvutie zaidi ili kufikia lengo la kuboreshwa kwa bustani hizo.

Alitoa ahadi hiyo alipokuwa akifungua rasmi bustani hiyo leo Juni 5, 2017 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kilele cha Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya ‘Nyerere Square’ Manispaa ya Dodoma.

Bustani hiyo inahudumiwa na Benki ya Biashara ya Akiba (ACB) kwa makubaliano maalum na Manispaa ya Dodoma, ambapo meneja wa tawi la Benki hiyo John Magigita imeeleza kuwa changomoto kubwa ni kuwabustani hiyo imezungukwa na wafanyabiashara ndogo hali inayopelekea kupoteza mvuto wake na kutoonekana vizuri.

Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede amesema Manispaa ya Dodoma itashirikiana na Ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya katika kuwahamisha wafanyabiashara hao na kutafutia nafasi katika masoko mengine baada ya soko la majengo kujaa hali iliyopelekea wao kupanga bidhaa zao katika viunga vya bustani hiyo.

Naye Ofisa Mazingira na Usafishaji wa Manispaa  ya Dodoma ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi katika Hafla hiyo fupi ya ufunguzi, alisema kuwa Manispaa imejipanga kuhakikisha mji wa Dodoma unakuwa katika hali ya usafi muda wote kwani tayari Dampo jipya la kisasa la kuzika taka lililopo katika eneo ya Chidaya limeshaanza kazi na kwamba watendaji wa Kata watashirikishwa kikamilifu katika kusimamia sheria za usafi na mazingira katika maeneo yao.


Thursday, May 25, 2017

MADIWANI MANISPAA YA DODOMA WAMPA KONGOLE RAIS MAGUFULI



Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme (kulia) akiongoza wimbo maalum wa kumsifu na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Magufuli kwa uamuzi wake wa kuifuta Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) Katikati ni Naibu Meya  wa Manispaa Dodoma Jumanne Ngede na kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi


Waheshimiwa Madiwani ambao ni wajumbe wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Dodoma  wakiimba wimbo maalum wa kumsifu na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Magufuli kwa uamuzi wake wa kuifuta Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) Wimbo huo ulikuwa ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Christina Mndeme (Hayupo pichani).



BARAZA la Madiwani wa Manispaa ya Dodoma limempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dokta John Magufuli kwa hatua  yake ya kuivunja rasmi iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao  Dodoma (CDA) na kwamba hatua ni maamuzi muhimu na sahihi kwa maendeleo  ya Manispaa na Mkoa wa Dodoma kwa ujumla.

Wajumbe wa Baraza hilo likiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye ni Naibu Meya  wa Manispaa hiyo Jumanne Ngede walikutana jana kwenye ukumbi wa Manispaa kwa ajili ya  Mkutano Maalum wa kuzungumza na vyombo vya Habari na kutoa  tamko rasmi la kumpongeza Rais Magufuli kwa hatua hiyo.

Walidai hatua hiyo itafungua milango kwa wawekezaji  wengi  kuwekea Dodoma kutokana  na taratibu za kupataji na umiliki wa ardhi kuboreshwa chini ya Manispaa, ikiwemo utolewaji wa hati za umiliki wa ardhi za miaka 99 badala zile za miaka 33 zilizokuwa zikitolewa na iliyokuwa CDA.


Mei 15 mwaka huu,  Mheshimiwa Rais Dokta John Magufuli alisaini tamko la Amri ya Rais la kuivunja iliyokuwa CDA baada ya kujiridhisha kuwa kwa sasa hakuna mahitaji ya kuwa na mamlaka hiyo iliyoanzishwa kwa Amri ya Rais mwaka 1973, na kwamba shughuli, mali, na watumishi 284 wanakuwa chini ya Manispaa ya Dodoma.

Wednesday, May 10, 2017

MALIASILI NA UTALII BLOG: BREAKING NEWS: TEMBO WANNE WAONEKANA CHUO KIKUU CH...: Tembo wakiwa wamejificha kwenye vichaka ndani ya eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) leo. Kwa mujibu wa taarifa za Wahifadhi wa Wanyama...

Friday, May 5, 2017

MADIWANI MANISPAA YA DODOMA WAMPONGEZA RAIS DOKTA MAGUFULI; WAPENDEKEZA CDA IVUNJWE


Katibu wa Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmshauri ya Manispaa ya Dodoma ambaye pia ndiye Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi (kushoto) akiwasilisha taarifa ya Katibu mbele ya wajumbe wa Baraza hilo katika Mkutano wa kawaida wa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2016/2017 jana katika ukumbi wa Manispaa. Kushoto kwake ni Naibu Meya wa Manispaa hiyo Jumanne Ngede   
Sehemu ya wajumbe wakifuatilia Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma katika Ukumbi wa Manispaa hiyo jana.
Diwani wa Kata ya Mtumba Manispaa ya Dodoma Edward Maboje akichangia taarifa iliyowasilishwa na Katibu wa Baraza la Madiwani la Manispaa hiyo Godwin Kunambi iliyojumuisha agizo la Rais Dokta John Magufuli kuhusu uongozi wa Mkoa na wadau wote kuchunguza na kuishauri Serikali endapo kuna haja ya kuendelea au kutoendelea kuwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao (CDA). Madiwani kwa ujumla wao wamependekeza Mamlaka hiyo ivunjwe.
Baadhi ya Wataalam wa Manispaa ya Dodoma wakifuatilia Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo katika Ukumbi wa Manispaa  jana. PICHA ZOTE: RAMADHANI JUMA

Na Ramadhani Juma
OFISI YA MKURUGENZI

MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma wameelezea kufurahishwa kwao na agizo alilotoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli kuhusu kuundwa kwa timu itakayokuwa na kujumu la kufanya kuchunguza na kuishauri Serikali endapo kuna haja ya kuendelea kuwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) katika kuendeleza mji wa Dodoma au jukumu hilo lifanywe na Halmashauri ya Manispaa kama ilivyo katika Manispaa zote nchini.

Wakichangia taarifa ya Katibu wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi ambaye pia ndiye Mkurugenzi wa Manispaa hiyo jana, wajumbe wa Baraza hilo walidai kuwa sasa imefikia wakati Mamlaka hiyo uvunjwe kwani imekuwa ikisababisha migogoro mingi ya ardhi badala ya kuupanga Mji huo kwani ndio jukumu lao la msingi.

Madiwani wote waliopata fursa ya kuchangia taarifa hiyo walieleza kuwa, wananchi wa Manispaa ya Dodoma wamechoshwa na uwepo wa Mamlaka ya CDA na kwamba imewanyanyasa kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuwapora ardhi zao bila kuzingatia sheria na taratibu.



Hivi karibuni Mheshimiwa Rais Dokta John Magufuli akiwa Mjini Dodoma aliagiza pamoja na mambo mengine, kufanywa majadiliano kati ya wadau ambao ni uongozi wa Mkoa, Mamlaka ya Ustawishaji (CDA), Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Wizara ya Ardhi na mamlaka zote zinazohusika ili ziiishauri Serikali juu ya umuhimu wa kuendelea au kutoendelea na Mamlaka ya hiyo.

Friday, April 28, 2017

HALMASHAURI ZAKARIBISHWA KUWEKEZA DODOMA




Meya wa Manispaa ya Kigamboni Mstahiki Maabad Hoja (wa pili kulia) na baadhi ya Madiwani na Wataalam wa Manispaa hiyo wakiwa katika ziara ya Mafunzo katika Dampo la Kisasa linalotumia  teknolojia  ya kuzika taka ngumu (Landa Fill) katika  Manispaa ya Dodoma jana Aprili 27, 2017. Wa kwanza kulia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede.
Meneja wa Dampo la Kisasa linalotumia  teknolojia  ya kuzika taka ngumu (Landa Fill) katika  Manispaa ya Dodoma John Chiwanga ( kushoto ) akitoa maelezo kwa Meya wa Manispaa ya Kigamboni Mstahiki Maabad Hoja (wa pili kulia) na baadhi ya Madiwani na Wataalam wa Manispaa hiyo walipokuwa katika ziara ya Mafunzo  jana Aprili 27, 2017. Wa kwanza kulia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede.

Mkuu wa Idara ya Usafi na Takangumu  Dickson Kimaro (aliyesimama) akitoa taarifa ya hali ya Usafi katika Manispaa ya Dodoma kwa Meya wa Manispaa ya Kigamboni Mstahiki Maabad Hoja (hayupo pichani) na baadhi ya Madiwani na Wataalam wa Manispaa hiyo walipokuwa katika ziara ya Mafunzo  jana Aprili 27, 2017. Waliokaa ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigamboni Rahel Muhando na Naibu Meya wa Manispaa hiyo Amini Sambo.

Mhandisi wa Mazingira wa Manispaa ya Dodoma Barnabas Faida (kulia) akitoa maelekezo kwa  Meya wa Manispaa ya Kigamboni Mstahiki Maabad Hoja (katikati) na baadhi ya Madiwani na Wataalam wa Manispaa hiyo walipokuwa katika ziara ya Mafunzo  jana Aprili 27, 2017, ya jinsi mashine za kupimia uzito wa taka ngunu inavyofanya kazi katika mzani uliopo kwenye Dampo la Kisasa linalotumia  teknolojia  ya kuzika taka ngumu (Landa Fill) katika  Manispaa ya Dodoma. PICHA ZOTE: RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI 


MKURUGENZI wa  Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi ametoa wito kwa Halmshauri nchini kuwekeza katika Manispaa ya Dodoma kama njia mojawapo ya kujiongezea mapato ya ndani.

Ametoa wito huo jana wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya mafunzo ya Madiwani na Wataalam wa Manispaa ya Kigamboni Mkoa wa Dar es Salaam waliyoifanya katika Manispaa ya Dodoma.

Kunambi aliwaeleza wageni  hao kuwa, Manispaa ya Dodoma ina fursa nyingi za uwekezaji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hoteli za kisasa, majengo ya Ofisi, na miundombinu mingine ikizingatiwa kuwa kuna rasilimali ardhi ya kutosha na sasa ni Makao Makuu ya Nchi.

Msafara wa watu 20 wakiwemo Madiwani na Wataalam kutoka Manispaa ya Kigamboni  ukiongozwa na Meya wa Manispaa hiyo Mstahiki  Maabad Hoja  walifanya ziara ya mafunzo juu ya usafi wa Mazingira na uhifadhi wa taka kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kuzika taka ardhini (Land Filling) ambapo Manispaa ya Dodoma inafanya vizuri kupitia Dampo lililopo katika Kata ya Ntyuka katika Manispaa hiyo.


Pia ziara yao ililenga kulijifunza kuhusu suala la utozaji na ukusanyaji wa kodi mbalimbali unaofanywa na Manispaa.

Friday, April 7, 2017

BANKI YA DUNIA YAKAGUA MIRADI MANISPAA YA DODOMA




 Mhandisi wa Mazingira Manispaa ya Dodoma Barnabas Faida (katikati) akifafanua jambo wakati wa ziara ya ukaguzi wa Dampo la kisasa la kuhifadhi taka ngumu iliyofanywa na maafisa kutoka  Benki ya Dunia jana Aprili 6, 2017.


Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia  (katikati) akishudia kazi ya kumwaga na kuhifadhi taka ngumu katika Dampo la kisasa lililopo Chidaya Manispaa ya Dodoma wakati yeye na ujumbe wake walipofanya ziara ya kukagua miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo jana April 6.  Wa pili Kulia  (mwenye suti) ni Mhandisi wa Ujenzi wa Manispaa ya Dodoma Lusako Kilembe na wa pili kushoto ni Mhandisi wa Mazingira Manispaa ya Dodoma Barnabas Faida. 

Kazi ya umwagaji na uhifadhi wa taka ngumu ikiendelea katika Dampo la Chidaya


Kazi ya umwagaji na uhifadhi wa taka ngumu ikiendelea katika Dampo la Chidaya.


Barabara ya 'Independence Square' ni miongoni miradi ya barabara za mji wa Dodoma iliyojengwa kwa kiwango cha lami kwa ufadhili wa Benki ya Dunia


TIMU ya maafisa kutoka Benki ya Dunia wamefanya ziara ya kukagua mradi  wa dampo la kisasa na Barabara zinazofadhiliwa na Benki hiyo katika Manispaa ya Dodoma chini ya Mradi wa Uimarishaji wa Miji Tanzania (TSCP).

Ziara hiyo ilifanyika jana April 6, 2017 ambapo timu hiyo ilitembelea eneo la Chidaya unakotekelezwa mradi wa dampo la kisasa linalotumia teknolojia ya kuzika taka (Land Fill) na kufurahishwa na maendeleo ya mradi ambao umeashaanza kufanya kazi huku ujenzi ukiwa katika hatua za mwisho.

Aidha ujumbe huo ulitembelea barabara zilizojengwa chini ya mradi huo unaotekelezwa katika Manispaa Saba Tanzania Bara pamoja na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).



Awali ujumbe huo ulikutana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi na kufanya nae mazungumzo mafupi, ambapo aliishukuru Benki ya Dunia kwa kusaidia kuboresha miundombinu katika Manispaa ya Dodoma huku akiiomba kuendelea kutoa ufadhili zaidi ili kuufanya mji wa Dodoma kuwa wa kisasa zaidi hivyo kuendana na hadhi yake ya kuwa makao makuu ya Nchi.



Monday, April 3, 2017

MEYA WA MANISPAA YA DODOMA AVULIWA MADARAKA

                                                                           

 Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede (wa pili kushoto) akizungumza wakati wa mkutano maalum cha Baraza la Madiwani wa Manispaa hiyo jana Aprili 3 ambapo uamuzi wa kumvua madaraka Meya wa Manispaa hiyo ulifikiwa. Kulia ni Mbunge wa dodoma Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu; Kazi Ajira na Vijana Mh. Anthony Mavunde na wa pili Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mh. Christina Mndeme. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi.

Wajumbe wakifuatilia mkutano



BARAZA la Madiwani wa Manispaa ya Dodoma limemvua madaraka Meya wa Manispaa hiyo Mstahiki Jaffar Mwanyemba kwa tuhuma za matumizi mabaya ya Ofisi yaliyopelekea upotevu wa shilingi milioni 30 za mradi wa Maji wa Kata ya Zuzu zilizotolewa na Serikali ya Japan kupitia ubalozi wake nchini Tanzania.

Hatua hiyo ilifikiwa katika mkutano wa dharura wa Bazara hilo ulioitishwa jana Aprili tatu katika ukumbi wa Manispaa ili  kupokea na kujadili taarifa ya Tume Maalum iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana kuchunguza tuhuma hizo.

Baada ya Katibu wa mkutano huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi kuwasilisha taarifa hiyo, wajumbe waliazimia kupiga kura ya kutokuwa na imani na Meya huyo, ambapo kati ya kura 48 zilizopigwa, kura 43 ziliunga mkono hoja hiyo huku kura 4 zikipinga na moja ikiharibika.


Kufuatia hali hiyo, Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede atakaimu nafasi ya Meya kwa mujibu wa Kanuni katika kipindi cha mpito kisichozidi siku 60, ambapo uchaguzi wa kumpata Meya mpya utafanywa.