Ramani ya Tanzania ikionesha Jiji la Dodoma lilipo kutoka katika Mikoa mingine yote ya Tanzania. |
..............................................................................
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma
imeongeza muda wa kulipia Viwanja kwa wateja wake wote walionunua Viwanja
kuanzia Aprili 20, mwaka huu kutoka siku 30 yaani Mwezi mmoja hadi siku 90
yaani miezi mitatu.
Aidha, Halmashauri hiyo
inatarajia kuendelea kuuza Viwanja vya eneo la Iyumbu kuanzia tarehe 5 Juni,
2018 kwani tayari imeshamaliza kazi ya kushughulikia malalamiko ya Wakazi wa
Ngaloni walioibuka na kudai kutolipwa fidia hapo awali.
Hayo yametangazwa na
Mkurugenzi wa Jiji hilo Godwin Kunambi wakati akiongea na Waandishi wa Habari
Jijini humo leo ambapo amesema Halmashauri imefikia uamuzi huo baada ya kuridhika
na mwenendo wa wateja kulipia Viwanja vyao ambapo mpaka sasa zaidi ya shilingi
bilioni 4 zimeshalipwa kwa Wananchi kama fidia ya maeneo yao yaliyotwaliwa
wakati wa upimaji.
Alitoa wito kwa wateja wote walionunua
viwanja na wanaoendelea kununua kutumia muda ulioongezwa kama fursa ya kukamilisha
malipo yao ili kuepuka usumbufu usio wa lazima baada ya muda huo kumalizika.
“Kwa wale wote waliokuwa
wanasubiri Viwanja vya Iyumbu wafike katika eneo letu la kuuzia Viwanja ambalo
ni Ofisi za Manispaa ya zamani jirani na Sabasaba siku ya tarehe 5 mwezi ujao…tutaanza
kuviuza siku hiyo” alisema Kunambi.
Katika hatua nyingine,
Mkurugenzi huyo wa Jiji ametoa muda wa miezi mitatu kwa watu wote waliopewa
Viwanja na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) katika maeneo ya
Njedengwa, Miganga, Mkonze, Iyumbu New Town Center, na Mkalama na hawajakamilisha
malipo ya Viwanja hivyo kukamilisha ndani ya kipindi hicho vinginevyo
Halmashauri itavitwaa kwa mujibu wa Sheria na kuviuza kwa wateja wengine wenye
mahitaji.
No comments:
Post a Comment