Thursday, May 24, 2018

‘VITA’ SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI YAZINDULIWA DODOMA


Mwanafunzi wa Kidato cha pili katika shule ya Sekondari ya Dodoma Huda Khalid Rabash akionesha kadi yake aliyokabidhiwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi (kushoto) kama ishara ya uzinduzi rasmi wa utoaji wa chanjo ya kinga dhidi ya ugonjwa wa Saratani ya Shingo ya kizazi kwa Wanawake. Kadi hiyo itamuwezesha kupata chanjo hiyo kwa awamu ya pili baada ya miezi sita ili kukamilisha kinga yake dhidi ya ugonjwa huo. Wengine wanaoshuhudia ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Hamadi Nyembea (mwenye miwani katikati nyuma)  na Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Amani Mfaume (mwenye miwani katikati mbele). Kushoto ni Mwalimu wa Afya wa Shule hiyo Caritas Burchard. PICHA ZOTE: RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI
Muhudumu wa Afya Ruth Azaliwa akimchoma Sindano ya chanjo dhidi ya Saratani ya Shingo ya Kizazi kwa Wanawake Mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Sekondari ya Dodoma Huda Khalid Rabash kuashiria uzinduzi wa zoezi la utoaji wa chanjo hiyo katika Wilaya ya Dodoma jana. Wanaoshuhudia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi (kushoto) na Mwalimu wa Afya wa Shule hiyo Caritas Burchard (kulia).
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi akimkabidhi kadi maalum kwa ajili kupata huduma ya chanjo awamu ya pili dhidi ya ugonjwa wa Saratani ya Shingo ya kizazi kwa Wanawake Mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Sekondari ya Dodoma Huda Khalid Rabash kama ishara ya uzinduzi wa zoezi la utoaji wa chanjo hiyo katika Wilaya ya Dodoma jana katika ukumbi wa Shule hiyo.  
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Hamadi Nyembea akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi la utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Saratani ya Shingo ya kizazi kwa Wasichana walio chini ya umri wa miaka 14 katika Wilaya ya Dodoma jana. Katikati ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi na wa kwanza ni Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Dodoma palikofanyika uzinduzi huo Mwalimu Amani Mfaume. 
Sehemu ya Wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari ya Dodoma wakifuatilia shughuli ya uzinduzi wa utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Saratani ya Shingo ya Kizazi  uliofanyika katika Shule hiyo jana.
Zoezi la utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Saratani ya Shingo ya kizazi kwa Wasichana walio chini ya umri wa miaka 14 likiendelea katika Sekondari ya Dodoma mara baada ya kuzinduliwa rasmi na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi.


................................................

ZOEZI la utoaji wa chanjo ya kinga dhidi ya ugonjwa wa Saratani ya Shingo ya Kizazi kwa Wanawake limezinduliwa rasmi katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma huku wasichana waliopatiwa chanjo hiyo wakitoa wito kwa wenzao kujitokeza na kuhakikisha wanakingwa dhidi ya ugonjwa huo.

Uzinduzi huo umefanyika jana katika ukumbi wa Dodoma Sekondari ambapo mgeni rasmi katika hafla fupi ya uzinduzi huo alikuwa Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi huku Mganga Mkuu wa Halmashauri Hamadi Nyembea akimwakilisha Mkurugenzi Godwin Kunambi.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kaimu Mkuu huyo wa Wilaya alisema uzinduzi huo ni kiashiria cha kuwafikia Wasichana wote wenye chini ya umri wa miaka 14 ndani ya Wilaya ya Dodoma.
Alisema zoezi hilo litaendeshwa na Halmashauri kupitia Ofisi ya Mganga Mkuu, na litashirikisha viongozi wa ngazi zote ikiwemo Kata na Mitaa ili kuhakikisha kila msichana anayehusika anafikiwa na kupatiwa chanjo hiyo.

Awali, Mganga Mkuu wa Halmashauri Hamadi Nyembea alisema katika kipindi cha Mwaka mmoja ujao, jumla ya Wasichana 7,828 walio na umri wa chini ya miaka 14 wanatarajiwa kufikiwa na kupatiwa chanjo hiyo katika Wilaya ya Dodoma.

Alisema  baada ya miezi sita Wasichana wote waliopatiwa chanjo hiyo watapatiwa tena kwa awamu ya pili ili kukamilisha kinga yao dhidi ya virusi vinavyoeneza ugonjwa huo.

Alimweleza Mgeni rasmi na wajumbe kuwa, chanjo hiyo imethibitishwa na Shirika la AfyaDuniani (WHO) hivyo Wasichana na Wazazi wasiwe na mashaka badala yake watoe ushirikiano wa kutosha ili kufikia lengo la Serikali la kutokomeza ugonjwa huo kama ilivyofanya kwa magonjwa kama Polio.

Tuesday, May 22, 2018

NAIBU WAZIRI LUGOLA APONGEZA UJENZI DAMPO LA KISASA


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Kangi Lugola (mwenye sare ya bluu) akipata maelezo jinsi mzani uliopo katika Dampo la kisasa la kuhifadhia taka lililopo Chidaya Manispaa ya Dodoma unavyofanya kazi kwa njia ya Kompyuta, kutoka kwa Mhandisi wa Mazingira wa Halmashauri hiyo Barnabs Faida.  
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Kangi Lugola (mwenye sare ya bluu) akifuatilia maelekezo ya jinsi maabara ya kupima kemikali kwenye maji ya ardhini katika eneo la Dampo la kisasa la Halmashauri ya  Manispaa ya Dodoma inavyofanya kazi ili kuhakikisha nuwepo wa Dampo hilo hauhatarishi vyanzo vya maji katika maeneo ya jirani. Anayetoa maelezo ni Afisa Mazingira kutoka Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka Ngumu ya Halmashauri hiyo  Happynes Pastory.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Kangi Lugola (wa tatu kushoto) akiwa katika eneo la Dampo la kisasa la kuhifadhia taka lililopo Chidaya Manispaa ya Dodoma alipofanya ziara kukagua Mifumo ya usimamizi wa Mazingira katika Dampo hilo inavyofanya kazi. Wa pili kushoto ni Diwani wa Kata ya Ntyuka Theobald Maina.
Sehemu ya Dampo iliyoanza kutumika
Sehemu ya pili ya Dampo ambayo itatumika baada ya sehemu ya kwanza kujaa

...................................................................

NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Kangi Lugola ameipongeza Halmashauri ya Manispaa Dodoma kwa ujenzi wa Dampo la kisasa la kuhifadhia taka kwa teknolojia ya kuzizika ardhini (Sanitary Land Fill) lililopo eneo la Chidaya Kata ya Matumbulu katika Halmashauri hiyo.

Alitoa pongezi hizo jana baada ya kufanya ziara katika Dampo hilo kwa lengo la kukagua mifumo ya usimamizi wa Mazingira.
“Mfikishieni Mkurugenzi wa Halmashauri salamu zangu…nimeridhika na uendeshaji wa Dampo hili na jinsi mnavyozingatia na kusimamia usalama wa Mazingira” alisema Naibu Waziri huyo.

Alisema ni fahari kubwa kwa Halamshauri ya Manispaa ya Dodoma kuwa na Miundombinu ya kisasa ya usafi na kutaka taka zote zinazozalishwa ziondolewe na kupelekwa katika Dampo hilo ili kufiki malengo ya mradi huo.

Dampo hilo lilianza kujengwa mwaka 2010 na hadi linakamilika limegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 7.1 ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Dunia kupitia Serikali Kuu ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa kuendeleza Miji ya Kimkakati Tanzania (TSCP) inayoratibiwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Naibu Waziri Lugola alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake ya siku saba katika Wilaya ya Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine, anakagua jinsi mifumo ya usimamizi wa Mazingira katika taasisi mbalimbali ikiwemo Hospitali na Vyuo inavyosimamiwa na kufanya kazi.


Friday, May 18, 2018

WAZIRI LUGOLA AANZA ZIARA YA WIKI MANISPAA YA DODOMA


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Kangi Lugola (wa pili kulia) akikagua mifumo ya usimamizi wa Mazingira katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma jana. Kushoto ni Afisa Mazingira wa Manispaa ya Dodoma Dickson Kimaro na pili kushoto ni Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mzee Nassoro. Wa tatu kutoka kulia ni Afisa Afya wa Mkoa wa Dodoma Carle Lyimo. PICHA ZOTE-RAMADHANI JUMA
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mzee Nassoro akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Kangi Lugola (katikati) wakati wa ziara ya kiongozi huyo katika hosptali hiyo jana.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Kangi Lugola (kulia) akikagua mifumo ya usimamizi wa Mazingira katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma jana. Kulia ni Afisa Afya wa Mkoa wa Dodoma Carle Lyimo.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Kangi Lugola akiwa katika sehemu ya Vyoo ya moja ya Wodi ya wagonjwa  akikagua mifumo ya usimamizi wa Mazingira katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma jana.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Kangi Lugola (kulia) akihakiki moja ya 'chemba' za mifumo ya maji katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu John wakati alipofanya ziara ya kukagua mifumo ya usimamizi wa Mazingira chuoni hapo jana.



..........................................................................


NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Kangi Lugola ameanza ziara ya kikazi ya wiki moja katika Manispaa ya Dodoma jana ambapo alitembelea Ofisi za Halmashauri na kupokea taarifa ya hali ya Mazingira kwa ujumla iliyowasilishwa na Mkuu wa Idara ya Mazingira na udhibiti wa taka ngumu Dickson Kimaro.

Naibu Waziri pia alipata taarifa kutoka kwa wataalam wa taasisi zingine ambazo ni wadau wa Mazingira ikiwemo Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Idara ya Madini, na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambao amefutana nao katika ziara hiyo.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake hapo jana, Naibu Waziri Lugola alitembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na Chuo Kikuu cha Mtakatifu John ambapo alikagua mifumo ya usimamizi wa taka ambapo kwa ujumla alikiri kuridhishwa jinsi taasisi hizo zinavyozingatia matakwa ya Sheria na taratibu za kuhifadhi Mazingira, lakini aliziagiza kuhakikisha takataka zinazoteketezwa kwa kuchomwa moto zinateketea kwa kiwango kinachokubalika.


Ziara ya Naibu Waziri inaendelea leo Ijumaa Mei 18, 2018 ambapo pamoja na maeneo mengine, atatembelea na kukagua mifumo ya usimamizi wa taka katika machinjio ya Punda iliyopo eneo la Kizota   na inatarajiwa kumalizika Mei 25, mwaka huu.     



Thursday, May 17, 2018

LAAC YA UGANDA ZIARANI DODOMA, YAFURAHIA MJI WA SERIAKLI


Mwakilishi wa Mkuu wa Idara ya Ujenzi wa Manispaa ya Dodoma Mhandisi Emanuel Manyanga akiwasilisha taarifa ya Miradi iliyotekelezwa na itakayotekelezwa kupitia Mradi wa Uendelezaji Miji ya Kimkakati Tanzanzia (TSCP) mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa ya Nchini Uganda ilipokuwa katika ziara ya kujifunza katika Manispaa hiyo jana. PICHA: OFISI YA MKURUGENZI
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa ya Nchini Uganda Reagan Okumu (kushoto) akizungumza wakati alipowaongoza wajumbe wa Kamati hiyo katika ziara ya kujifunza katika Manispaa ya Dodoma jana.
Mhandisi wa Mazingira wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Barnabas Faida akitoa neno la utangulizi kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesbu za Srikali za Mitaa ya Uganda ilipotembelea Halmashauri hiyo jana.
WAJUMBE wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa ya Bunge la Uganda wakifuatilia taarifa za miradi ya Ujenzi iliyokuwa akiwasilishwa na Mhandisi Emanuel Manyanga kutoka Idara ya Ujenzi ya Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma walipofanya ziara ya kujifunza juu ya utekelezaji wa miradi ya Kimkakati. 

............................................................

WAJUMBE wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa ya Bunge la Uganda wameishukuru Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kwa kuipatia Serikali ya Nchi hiyo kiwanja chenye ukubwa wa eka tano katika Kata ya Mtumba eneo utakapojengwa Mji wa Serikali.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Reagan Okumu alitoa Shukrani hizo jana wakati Kamati hiyo ilipotembelea Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma walipokuwa katika ziara ya siku moja ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama Dampo la kisasa la kuhifadhia taka kwa kuzifukia ardhini (Sanitary Land Fill) lililopo Kata ya Matumbulu ambalo ni moja ya miradi mikubwa katika eneo la usafi na utunzaji wa mazingira.

Awali akizungumza mbele ya Kamati hiyo, Mhandisi wa Mazingira wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Godwin Kunambi, aliwajulisha wajumbe hao kuwa, Halmashauri imetenga na kupima eneo litakalojengwa Mji wa Serikali hapa Dodoma na kwamba Serikali ya Uganda imepewa kiwanja chenye ukubwa wa eka tano kwa ajili ya matumizi ya kiofisi, ambapo pia walioneshwa ramani ya eneo hilo.

Wajumbe wa Kamati hiyo waliezea kufurahishwa kwao na hatua hiyo huku wakiahidi kufikisha taarifa hizo njema kwa Wananchi wa Uganda mara watakaporejea Nchini humo.
   

Saturday, April 28, 2018

MADIWANI MWANZA WAWEKA HISTORIA JIJINI DODOMA

Diwani wa Kata ya Nyamagana Jijini Mwanza ambaye pia ni Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji hilo Mhe. Bhiku Kotecha (wa pili kushoto-mbele) akiwa na baadhi ya Madiwani na Wataalam wa Halmashauri hiyo walipotembelea Dampo la kisasa la kuhifadhia takataka lililopo eneo la Chidaya Jijini Dodoma jana. Mbele kushoto ni Mhandisi wa Mazingira wa Jiji la Dodoma Barnabas Faida na kulia ni Afisa Habari wa Jiji la Mwanza Martin Sawema. PICHA:DCC
Mhandisi wa Mazingira wa Jiji la Dodoma Barnabas Faida na (kuhoto) akitoa maelezo kuhusu mradi wa Dampo la kisasa la Chidaya kwa Madiwani na Wataalam wa Jiji la Mwanza waliotembelea eneo hilo jana Aprili 27, 2018 kwa lengo la kujifunza. 


Operesheni za kuhifadhi takataka zikiendelea katika Dampo la kisasa la Chidaya Jijini Dodoma.
Mhandisi wa Mazingira wa Jiji la Dodoma Barnabas Faida na (kuhoto) akifuatilia  maswali kuhusu mradi wa Dampo la kisasa la Chidaya kutoka kwa Madiwani na Wataalam wa Jiji la Mwanza waliotembelea eneo hilo jana Aprili 27, 2018 kwa lengo la kujifunza. 
Muonekano wa sehemu ya Dampo la kisasa la Chidaya Jijini Dodoma ambayo bado haijaanza kutumika.


................................................................
MADIWANI wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wameingia kwenye historia ya kuwa wageni wa kwanza kufanya ziara ya kubadilishana uzoefu katika Halmashauri ya Jiji jipya la Dodoma mara baada ya iliyokuwa Manispaa ya Dodoma kupandishwa hadhi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Magufuli wakati wa Sherehe za miaka 54 ya Muungano Aprili 26, mwaka huu zilizofanyika katika uwanja ya Jamhuri Jijini humo.

Madiwani hao wa jiji la Mwanza wakiongozwa na Naibu Meya Mhe. Bhiku Kotecha ambaye ni Diwani wa Kata ya Nyamagana, walitembelea Halmashauri ya Jiji la Dodoma jana Aprili 27, 2018 ikiwa ni siku moja tangu iliyokuwa Manispaa ya Dodoma kupewa hadhi ya Jiji.

Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kubadilishana uzoefu hususan katika suala la Usafi wa Mazingira, ambapo walitembelea Dampo la kisasa la kuhifadhia takataka kwa njia ya kuzifukia (Sanitary Land Fill) lililopo eneo la Chidaya Kata ya Matumbulu nje kidogo ya Jiji la Dodoma.

Wakiwa katika eneo la Dampo, walipata maelezo ya kina juu ya mradi huo kutoka kwa Mhandisi wa Mazingira wa Jiji la Dodoma Barnabas Faida, ambaye aliwaeleza kuwa, mradi huo umetekelezwa kwa awamu kuanzia mwaka 2011 kwa Fedha za Serikali Kuu ikiwa ni mkopo wa Benki ya Duniani kupitia mradi wa kuimarisha Majiji ya Kimkakati (TSCP) na kwamba hadi kukamilika kwake umegharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 7.1, huku ukiwa tayari umeanza kufanya kazi.


Monday, April 23, 2018

KAZI YA UUZAJI WA VIWANJA 10,864 YAZIDI KUSHIKA KASI


Wateja wakieleweshwa eneo vilipo viwanja
Wateja wakiwa katika eneo maalum la kupumzikia wakati wakiendelea na taratibu za ununuzi wa viwanja

Mkuu wa Idara ya Ardhi Mipango Miji na Maliasili Joseph Mafuru (katikati) akishughulikia changamoto ya mteja.

..........................................
KAZI ya uuzaji wa Viwanja 10,684 imeendelea leo Jumatatu Aprili 23, 2018 katika eneo la Ofisi Kuu ya zamani ya Manispaa zilizopo jirani na Sabasaba.

Zoezi hilo lilianza siku ya Ijumaa Aprili 20, 2018, ambapo jumla ya wateja 399 walipatiwa Viwanja kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Katika awamu ya kwanza leo, wateja wapatao 400 wanaotarajiwa kuhudumiwa wamepatiwa kuponi za namba ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa kuhudumiwa.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Ardhi Mipango Miji na Maliasili Joseph Mafuru, zoezi la uuzaji wa Viwanja litaendelea mpaka Viwanja vyote vitakapomalizika na kwamba Wananchi wote wanakaribishwa.